Madiwani, wenyeviti vijiji watishia Kigoma kujitoa NCCR-Mageuzi


Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, akihutubia mamia ya wananchi katika Kijiji cha Nguruka wilayani Kigoma ikiwa ni mkutano wake wa kwanza tangu chama chake cha NCCR-Mageuzi kilipotangaza kumvua uanachama.

Baadhi ya madiwani, wenyeviti wa serikali za vijiji kupitia NCCR Mageuzi katika Jimbo la Kigoma Kusini pamoja na wanachama, wamesema watajiuzulu nyadhifa zao zote za serikali na kurudisha kadi za chama hicho ikiwa mbunge wa jimbo hilo, David Kafulila, atavuliwa uanachama na kupoteza ubunge.

Walitoa tamko hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Nguruka, wilayani Kigoma, baada ya kumkaribisha Kafulila na makamishna wa NCCR-Mageuzi kutoka mikoa ya Kigoma, Ruvuma na Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti hao wa vijiji, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyangabo, Kata ya Nguruka, Simon Katenza, alisema hawakubaliani na hatua iliyochukuliwa na Halmashauri Kuu (NEC) ya NCCR-Mageuzi ya kumvua uanachama mbunge wao.

“Mheshimiwa mbunge, utambue kuwa sisi wenyeviti wa vijiji na vitongoji tuko nyuma yako. Hatukubaliani na hili. Na ikiwa unapoteza ubunge basi tutakwenda wote utakakoelekea. Haiwezekani uchaguliwe na maelfu ya watu eti watu wasiozidi hamsini waje wakuondoe. Hatukubaliani,” alisema.

Diwani wa Kata ya Kandaga, Francis Kumbo, alisema wako tayari kuachia madaraka waliyonayo ikiwa hatua ya kumvua uanachama Kafulila itafikiwa na kwamba wamesikitishwa na hatua ya chama hicho chenye mizizi katika jimbo hilo kutowasikiliza wananchi wanasemaje juu ya mbunge wao.

Katika Jimbo la Kigoma Kusini, NCCR-Mageuzi inaongoza vijiji nane na ina madiwani wanne katika Kata za Nguruka, Itebula, Mganza na Kandaga.

Naye Kamishna wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Kigoma, Bakari Nyamcha, alisema ikiwa Kafulila atavuliwa uanachama atatembea mkoa mzima kuhakikisha chama hicho kinafutika.

Nyamcha ambaye ni mjumbe wa NEC alisema wamefanya kazi kubwa kuhakikisha chama kinapata wabunge mkoani, lakini juhudi zao zinaonekana ni balaa kwenye NCCR-Mageuzi hivyo kuliko kuendelea kuwa kwenye chama hicho ni bora kikafutika na kwa kuwa wao ndio wamekuwa wakifanya kazi ya kukieneza chama siku zote watapita kila kijiji kukifuta na kuwapa wafuasi wao mwelekeo mpya.

Akihutubia maelfu ya wananchi katika viwanja hivyo, Kafulila ambaye aliingia kwa maandamano, aliwaambia wananchi kuwa pamoja na kuomba radhi kwa mdomo na maandishi hakusikilizwa na ndio sababu alikwenda mahakamani kwa kuwa hakukuwa na namna nyingine ya kufanya katika kulipatia ufumbuzi suala hilo.

“Ndugu wananchi, kwa suala hili liko mahakamani na sipendi kuingilia uhuru wa mahakama. Lakini nilifanya jitihada za kuhakikisha mnaendelea kuwa na mwakilishi baada ya uamuzi wa Halmashauri Kuu. Lakini sikusikilizwa. Hivyo njia pekee ya kulinda kura zenu mlizonipa mwaka juzi ni kwenda mahakamani,” alisema Kafulila.

Aliongeza: “Tunataka kura za wananchi ziheshimiwe. Hivyo. mahakama ilitoa uamuzi wa chama kutoendelea na hatua zaidi dhidi yangu. Kwa hiyo, mimi bado ni mbunge, nitaendelea kutimiza majukumu yangu kama mbunge. Hivyo, msiwe na hofu wala mashaka,” alisema kafulila.

Alisema pamoja na kesi iliyoko mahakamani, baadhi ya wananchi wa jimbo hilo wiki hii watafungua kesi nyingine ya kikatiba juu ya suala hili.

“Hivi tunavyoongea, baadhi ya wananchi wako Dar es salaam. Watafungua kesi na hii itakuwa ya kihistoria. Kwa kuwa itakuwa kesi ya kwanza. Suala kubwa ni kuona inakuwaje kiongozi anachaguliwa na maelfu ya watu halafu watu wachache wanaweza kukaa na kumwondoa bila hata waliomchagua kujulishwa wala kushirikishwa,” alisema Kafulila.

Katika mkutano huo, Kafulila aliambatana na Kamishna wa Mkoa wa Ruvuma, Henri Mapunda, na Kamishna wa Mkoa wa Dodoma, Kayumbo Kabutari, ambao walipewa karipio kali na NEC ya chama hicho wakati Kafulila na wenzake walivuliwa uanachama.

Makamishna hao walieleza katika mkutano huo kuwa kudai haki kumewaponza, lakini wataendelea kufanya hivyo hadi chama kitakapokuwa katika misingi imara.

Leave a Comment