Kuendelea operesheni za jeshi la Mauritania dhidi ya tawi la al Qaida Kaskazini mwa Afrika


Askari wa jeshi la Mauritania wamewaangamiza wafuasi 15 wa kundi la al-Qaeda in the Islamic Maghreb AQIM, katika operesheni za kutokomeza wafuasi wa kundi hilo. Operesheni hiyo imefanyika katika eneo la Wagadou lililoko katika mpaka wa Mauritania na Mali.

Jeshi la Mali pia limewakamata watu 9 wanaotuhumiwa kushirikiana na kundi hilo, 6 kati ya watuhumiwa hao ni Wamauritania na watatu wanatoka katika kabila la Fulani.

Duru za kijeshi zinatabiri kwamba, viongozi wa kundi hilo la wanamgambo la AQIM, wanakusudia kuasisi ngome mpya katika eneo hilo la msituni la Wagadou lililoko magharibi mwa Mali.

 

Askari wa jeshi la Mauritania wanasaidiana na wanajeshi wa Mali katika operesheni hizo za kuwasaka na kuwatokomeza wanamgambo wa kundi hilo. Kundi la wanamgambo wa al-Qaeda in the Islamic Maghreb AQIM ambalo ngome yake kuu ipo nchini Algeria, limeanzisha kambi katika nchi ya Mali zinazozitumiwa katika mashambulizi ya silaha na utekaji njara raia wa kigeni kwenye eneo la Jangwa la Sahara.

Baada ya vikosi jeshi la Mauritania kuondoka Mali miezi miwili iliyopita, kundi la AQIM lilianzisha vituo viwili vipya katika mpaka wa nchi hizo mbili. Kwa sababu hiyo, wanajeshi wa nchi hizo mbili jirani mwanzoni mwa mwezi huu wa Juni walikubaliana kufanya operesheni za pamoja dhidi ya ngome na vituo vya kundi hilo.

Nchi za Algeria, Mali, Mauritania na Niger ambazo ndizo zinazolengwa zaidi kwa mashambulizi ya kundi la wanamgambo wa AQIM zinashirikiana kwa karibu katika masuala ya kijeshi na kiusalama katika jitihada za kukomesha mashambulizi na shughuli za kundi hilo.

Mashambulizi ya kwanza ya silaha ya kundi la AQIM yalifanywa mwaka 2006 nchini Mauritania.

Mfano mwingine wa shughuli za kigaidi za kundi hilo ni mlipuko wa bomu la kujitolea mhanga uliotokea mwezi Agosti miaka miwili iliyopita karibu na ubalozi wa Ufaransa katika mji mkuu wa Mauritania Nouakchott.

Wafuasi wa kundi hilo pia wanawateka njara raia wa kigeni hasa wa nchi za Ulaya pamoja na kushiriki katika biashara haramu ya silaha na magendo ya madawa ya kulevya katika eneo hilo.

Leave a Comment