UKIMWI


UKIMWI

Karibuni katika sehemu hii nyingine ya mfululizo wa makala za Ijue Afya Yako ambapo hapa tutajadili kwa ufupi kuhusu ugonjwa angamizi wa UKIMWI. Kama mnavyojua hadi hii leo haujapata tiba licha ya juhudi kubwa za wataalamu kutoka pembe mbalimbali duniani za kutafuta tiba dhidi ya maradhi hayo. *************************
HIV ni ufupisho wa Human Immuno Deficiency Virus yaani kirusi kinachodhoofisha kinga ya mwili na kuufanya mwili ushindwe kukabiliana na magonjwa na hatimaye kusababisha ukimwi. Imeelezwa kuwa urahisi wa safari za kimataifa umekuwa moja ya sababu kubwa za uambukizaji wa haraka wa HIV. Wasafiri wanakadiriwa kuwa na uwezekano wa kuambukizwa virusi vya HIV mara 200 zaidi wakiwa nje ya nchi zao, kuliko wakiwa nchini kwao. Hapa inatupasa kwanza kujiuliza swali muhimu ambalo ni:
Ukimwi husababishwa na nini?
Ugonjwa wa ukimwi husababishwa na kirusi cha HIV. Kirusi hiki hushambulia kinga ya mwili na hivyo kuufanya ushindwe kukabiliana na magonjwa mbalimbali. Inaweza kuchukua miaka mingi kwa dalili za ugonjwa huo kuanza kujitokeza baada ya kuambukizwa virusi hivyo. Kwa msingi huo hiyo siha na uzima wa kidhahiri wa mwili wa mtu haumaanishi kuwa mtu huyo hajaambukizwa virus vya HIV.
Virusi vya ukimwi vinaambukizwaje?
Ni vyema kwanza tufahamu njia zinazosababisha na kueneza maambukizo ya ugonjwa huu hatari wa ukimwi, kabla ya kuzungumzia dalili zake.
Ugonjwa huu umeziathiri na bado unaendelea kuziathiri kwa kiasi kikubwa nchi nyingi za ulimwengu wa tatu. Utafiti unaonyesha kuwa, sababu kuu zinasosababisha maambukizo ya ukimwi ni hizi zifuatazo:
1. Kufanyaji ngono bila ya kutumia kinga, khususan mipira ya kondom.
2. maambukizo kutoka kwa mama hadi kwa mtoto wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na wakati wa kunyonyesha
3. Uchangiaji wa damu. Kwa mfano Wakati mtu anapotoa damu kumpa mwingine bila ya kupimwa ipasavyo na kuhakikisha kuwa damu hiyo ni salama.
4. Vitendo vya kuchangia vifaa na suhula zinazotumika katika kutoboa ngozi, vifaa vya kutogea masikio, pua, kutahiri na kadhalika. Kuchangia vifaa na zana hizo bila ya kusafishwa na kutakaswa kwa kutumia njia salama za kiafya au Sterilization.
5. Kusuguana ngozi yenye michubuko na damu yenye maambukizi na majimaji ya mwili.
6. Uchangiaji wa sindano moja ya madawa ya kulevya kwa watu kadhaa, nk .
Sasa umewadia wakati wqa kuzungumzia dalili za ugonjwa wa Ukimwi ambazo ni hizi zifusatazo:
Kwanza ni kudhoofika kwa mwili na kupungua uzito kwa asilimia kumi au zaidi, homa za mara kwa mara, kuharisha mfululizo kwa zaidi ya wiki nne, vidonda sehemu za siri na mdomoni, kuvimba tezi, majipu mwili mzima, saratani au kansa ya ngozi, utando mweupe mdomoni, ukurutu n .k.
Itafahamika kuwa baada ya virusi vya ukimwi kuangamiza kinga ya mwili, yaani chembe chembe hai nyeupe za damu, uwezo wa mwili wa kupambana na magonjwa hupungua. Kwa hiyo ni wazi kuwa katika kipindi hicho mwili unaweza kushambuliwa na magonjwa mbalimbali na kushindwa kukabiliana nayo.
Swali nyingine muhimu la kuulizwa hapa ni kuwa je, Kuenea kwa virusi vya ukimwi kunasababishwa haswa na tabia zipi? Ni vyema tufahamu sababu zinazochangia kuenea kwa virusi vya ukimwi katika jamii zetu ili tuweze kuepukane na ugonjwa huo hatari.
Virusi vya ukimwi vinaenea kwa kiwango kikubwa kwa njia ya kujamiina. Kujaaminiana huko ni kwa aina gani. Mtu anapotoka nje ya ndoa ovyo ovyo na na kujihusisha na vitendo vya ngono na watu wengi, uwezekano wa kuambukizwa ugonjwa huo unaongezeka, kwa kuwa kila mmoja miongoni mwa watu hao yumkini akawa chanzo cha kupata virusi hivyo.-
Vile vile mtu akifanya tendo la kujamiiyana kwa njia isiyo salama, kwa maana ya kuingiliana kimwili bila ya kutumia kondomu, anahatarisha maisha yake.
Sababu nyingine pia inayoeneza virusi vya ukimwi ni kuchelewa kutibu magonjwa ya zinaa. Hiyo nayo inachangia kuenea kwa virusi vya ukimwi. Kwani mtu anapougua ugonjwa wa zinaa, virusi vya ukimwi vinaweza kumshambulia na kuingia mwilini kwa urahisi zaidi kutokana na vidonda alivyonavyo katika sehemu zake za siri. Matumizi ya madawa ya kulevya pamoja na pombe huchangia vile vile kuchukua maamuzi yasiyo sahihi na kumshajiisha mtu kufanya matendo ya ngono. Tunaendelea mbele na kipindi chetu cha Ijue Afya Yako kwa kutupia jicho njia zisizoweza kusabababisha maambukizo ya virusi vya ukimwi hususan ikizingatiwa kwamba kumekuwepo na dhana kwamba kuishi au kuwa karibu na muathirika wa virusi humfanya mtu kukumbwa na ugonjwa huo haraka ka njia hiyo baadhi ya familia zimekuwa zikiwatenga waathirika kwa dhana hiyo potofu. Kuna njia kadha wa kadha ambazo hazienezi virusi vya ukimwi. Lakini hapa nitataja hizi zifuatazo: Kula chakula katika chombo kimoja na mtu mwenye ukimwi, kuchangia choo kimoja, kupiga chafya kwa mgonjwa wa ukimwi, na kumshumu mashavuni mtu mwenye virusi vya ukimwi. Yote hayo hayasababishio maambukizi ya virusi hivyo.
Ushahidi unaonyesha kuwa juhudi za kupambana na gonjwa angamizi la ukimwi zinaweza kuzaa matunda, iwapo juhudi hizo zitapanliwa zaidi katika nchi zilizoathiriwa kwa kiasi kikubwa na ukimwi. Kwanza kabisa ni kwa kupanua kampeni za kuzuia maambukizo ya ukimwi na kuepuka zinaa kwa kuheshimu sheria za dini. Kuepuka ngono zembe na kuamianiana katika ndoa. Kutumia mipira ya kujikinga na ukimwi au kondomu. Kupima kwa hiari na kuona iwapo damu yako imeathirika na ukimwi au la. Kwani iwapo mtu atafahamu kuwa ana virusi vya ukimwi, anaweza kuepusha maambukizo kwa watu wengine. Vile vile kupitia upimaji wa khiari, muathirika huelimishwa namna ya kupata matibabu na msaada utakomuwezesha kuishi kwa kufuata misingi ya kiafya. Na wale ambao watakutwa hawajaathirika katika vipimo vyao, wanaweza kubadili tabia na mienendo yao na hivyo kujiepusha na kutumbukia kwenye gonjwa hilo hatari. Maambukizo ya mama kwa mtoto yanaweza kuzuiwa kwa kupima damu ya mama ili kufahamu iwapo ameambukizwa au la. Iwapo mama mwenye virusi vya HIV atapewa dawa za kudhoofisha nguvu za virusi vya ukimwi, hatua hiyo hupunguza hatari ya kumuambukizwa mtoto wake atakayezaliwa kwa kiasi kikubwa. Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani WHO umethibitisha kuwa utoaji wa dawa kuzuia maambukizo ya ukimwi kutoka kwa mama hadi kwa mtoto umefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika nchi za ulimwengu wa tatu. Tunapenda kusisitiza tena kuwa hadi hivi sasa na licha ya juhudi chungu nzima za wasomi na wataalamu wa kiafya kutoka pembe mbalimbali za dunia kutafuta tiba ya kutokomeza ugonjwa wa ukimwi, lakini hadi sasa wameshinda kupata tiba kamili ya ugonjwa huo uliokwisha angamiza mamilioni ya watu na ukiendelea kuwa tishio kwa walimwengu khususan katika msabara ya Afrika na Asia. Madawa yanayotumika hivi sasa ni yale ya ARV’s ambayo hudhoofisha kufifiza ukuaji wa virusi vya HIV mwilini na hivyo kuongeza muda wa maisha ya muathirika.
Kwa hakika kuna mengi ya kuzungumza kuhusiana na ugonjwa hatari wa ukimwi hata hivyo ni vyema tuishie hapa kwa leo. N imatumaini yangu kuwa mumenufaika na yale yote niliyoweza kukuandalieni katika makala hii. Tunakaribisha maoni na mapendekezo. Tafadhali soma makala nyingnezo za mfululizo huu wa “Ijue Afya Yako” kwa faida yako na kwa ajili ya kuwafaidisha wengine. Kama una ushauri wowote tafadhali tuandikie: swahiliradio@irib.ir .

2 Comments

  1. tobiasy says:

    nasshukuru sana kwa mafunzo mliyotuletea na kwa kweli yanasaidia sana. ila pamoja na hayo ninaomba niulize swali ambalo kwa kweli sijalielewa vizuri. JE VIRUSI VYA UKIMWI HUCHUKUA MUDA GANI KUSAMBAA MWILINI ENDAPO DAMU INAYOTOKEA KWENYE MAJERAHA YA WAWILI HAWA ITAINGILIANA.???

Leave a Comment